5:1 Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng`ambo ya ziwa.
5:2 Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye.
5:3 Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo.
5:4 Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia.
5:5 Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe.
5:6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia
5:7 akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!"
5:8 Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.")
5:9 Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni `Jeshi`, maana sisi tu wengi."
5:10 Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile.
5:11 Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima.
5:12 Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie."
5:13 Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini.
5:14 Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia.
5:15 Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa.
5:16 Watu walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe.
5:17 Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao.
5:18 Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye.
5:19 Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma."
5:20 Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa.
5:21 Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa.
5:22 Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake,
5:23 akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi."
5:24 Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande.
5:25 Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili.
5:26 Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya.
5:27 Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake.
5:28 Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi lake, nitapona."
5:29 Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake.
5:30 Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi yangu?"
5:31 Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?"
5:32 Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo.
5:33 Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote.
5:34 Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako."
5:35 Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?"
5:36 Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu."
5:37 Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo.
5:38 Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi.
5:40 Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana.
5:41 Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!"
5:42 Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi.
5:43 Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.