4:1 Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi.
4:2 Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu.
4:3 Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa.
4:4 Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima,
4:5 na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu.
4:6 Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo.
4:7 Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu.
4:8 Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu.
4:9 Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana.
4:10 Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi.
4:11 Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali.
4:12 Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.
4:13 Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini.
4:14 Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.
4:15 Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia.
4:16 Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza.
4:17 Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana.