3:1 Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.
3:2 watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu;
3:3 watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;
3:4 watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
3:5 Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.
3:6 Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina;
3:7 wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli.
3:8 Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose.
3:9 Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.
3:10 Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu,
3:11 udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote.
3:12 Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe.
3:13 Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe.
3:14 Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako.
3:15 Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu.
3:16 Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili,