5:1 Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana ninyi ni watoto wake wapenzi.
5:2 Upendo uongoze maisha yenu, kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama dhabihu yenye harufu nzuri na tambiko impendezayo Mungu.
5:3 Kwa vile ninyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu.
5:4 Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa.
5:5 Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mfisadi, (ufisadi ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika Utawala wa Kristo na wa Mungu.
5:6 Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii.
5:7 Basi, msishirikiane nao.
5:8 Zamani ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga:
5:9 maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli.
5:10 Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana.
5:11 Msishiriki katika matendo yasiyofaa, ya giza bali yafichueni.
5:12 Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja.
5:13 Lakini mambo yale yanayotendwa katika mwanga, ukweli wake hudhihirishwa;
5:14 na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: "Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka wafu, naye Kristo atakuangaza."
5:15 Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi: Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima.
5:16 Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya.
5:17 Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana.
5:18 Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu.
5:19 Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu.
5:20 Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
5:21 Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya kumcha Kristo.
5:22 Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana.
5:23 Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake.
5:24 Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote.
5:25 Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake.
5:26 Alifanya hivyo, ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji,
5:27 kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safu kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo.
5:28 Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. ((
5:29 Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa,
5:30 maana sisi ni viungo vya mwili wake.)
5:31 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa hiyo, mwanamume atawaacha baba na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja."
5:32 Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake.
5:33 Lakini yanawahusu ninyi pia: kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.