6:1 Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa.
6:2 Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.
6:3 Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.
6:4 Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine.
6:5 Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba.
6:6 Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
6:7 Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.
6:8 Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.
6:9 Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.
6:10 Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
6:11 Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.
6:12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.
6:14 Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.
6:15 Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.
6:16 Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu.
6:17 Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.