2:1 Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe.
2:2 Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.
2:3 Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu,"
2:4 je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
2:5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda.
2:6 Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani?
2:7 Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?
2:8 Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa.
2:9 Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia.
2:10 Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote.
2:11 Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria.
2:12 Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.
2:13 Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.
2:14 Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?
2:15 Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula.
2:16 Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?
2:17 Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
2:18 Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu.
2:19 Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu.
2:20 Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa?
2:21 Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu.
2:22 Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake.
2:23 Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu."
2:24 Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake.
2:25 Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.
2:26 Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.