Bad Advertisement?

News / Reviews:
  • World News
  • Movie Reviews
  • Book Search

    Are you a Christian?

    Online Store:
  • Visit Our eBay Store



  • SWAHILI BIBLIA - JOHN 7

    JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


    7:1 Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumwua.

    7:2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

    7:3 Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya.

    7:4 Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadam unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu."

    7:5 Hata ndugu zake hawakumwamini!)

    7:6 Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa.

    7:7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu.

    7:8 Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika."

    7:9 Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.

    7:10 Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.

    7:11 Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza: "Yuko wapi?"

    7:12 Kulikuwa na minong`ono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, "Ni mtu mwema." Wengine walisema, "La! Anawapotosha watu."

    7:13 Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.

    7:14 Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza kufundisha.

    7:15 Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?"

    7:16 Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.

    7:17 Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.

    7:18 Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.

    7:19 Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?"

    7:20 Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?"

    7:21 Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.

    7:22 Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato.

    7:23 Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato?

    7:24 Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki."

    7:25 Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu?

    7:26 Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?

    7:27 Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!"

    7:28 Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, "Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.

    7:29 Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma."

    7:30 Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.

    7:31 Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, "Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?"

    7:32 Mafarisayo waliwasikia watu wakinong`ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.

    7:33 Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma.

    7:34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika."

    7:35 Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?

    7:36 Ana maana gani anaposema: `Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?"`

    7:37 Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe.

    7:38 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: `Anayeniamini mimi, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!"`

    7:39 Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.)

    7:40 Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!"

    7:41 Wengine wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema, "Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya?

    7:42 Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: `Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!"`

    7:43 Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.

    7:44 Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.

    7:45 Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, "Kwa nini hamkumleta?"

    7:46 Walinzi wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!"

    7:47 Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika?

    7:48 Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini?

    7:49 Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!"

    7:50 Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia,

    7:51 "Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?"

    7:52 Nao wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!" [[[

    7:53 Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda zake;

    IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

    God Rules.NET
    Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine