1:1 Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.
1:2 Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.
1:3 Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,
1:4 ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
1:5 Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.
1:6 Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.
1:7 Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
1:8 Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,
1:9 Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.
1:10 Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.
1:11 Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.
1:13 Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
1:14 Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
1:15 Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
1:16 Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
1:17 Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake."
1:18 Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu."
1:19 Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema.
1:20 Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia."
1:21 Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni.
1:22 Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
1:23 Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.
1:24 Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema:
1:25 "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu."
1:26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya,
1:27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi.
1:29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini?
1:30 Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.
1:31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu.
1:32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake.
1:33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho."
1:34 Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?"
1:35 Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.
1:36 Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
1:37 Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu."
1:38 Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.
1:39 Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda.
1:40 Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
1:41 Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
1:42 akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.
1:43 Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
1:44 Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
1:45 Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia."
1:46 Naye Maria akasema,
1:47 "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
1:48 Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
1:49 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
1:50 Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
1:51 Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
1:52 amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
1:53 Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
1:54 Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
1:55 Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."
1:56 Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
1:57 Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
1:58 Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
1:59 Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya.
1:60 Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane."
1:61 Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?"
1:62 Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
1:63 Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu.
1:64 Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
1:65 Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.
1:66 Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
1:67 Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:
1:68 "Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake.
1:69 Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.
1:70 Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu,
1:71 kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
1:72 Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.
1:73 Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi
1:74 tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,
1:75 kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.
1:76 Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
1:77 kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.
1:78 Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu,
1:79 na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani."
1:80 Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.