19:1 Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo.
19:2 Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.
19:3 Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.
19:4 Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.
19:5 Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako."
19:6 Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.
19:7 Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung`unika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi."
19:8 Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang`anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne."
19:9 Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.
19:10 Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea." ic
19:11 Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.)
19:12 Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi.
19:13 Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: `Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.`
19:14 Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: `Hatumtaki huyu atutawale.`
19:15 "Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.
19:16 Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.`
19:17 Naye akamwambia: `Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!`
19:18 Mtumishi wa pili akaja, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.`
19:19 Naye akamwambia pia: `Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.`
19:20 "Mtumishi mwingine akaja, akasema: `Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,
19:21 kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.`
19:22 Naye akamwambia: `Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.
19:23 Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?`
19:24 Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: `Mnyang`anyeni hizo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.`
19:25 Nao wakamwambia: `Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!`
19:26 Naye akawajibu: `Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
19:27 Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."`
19:28 Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.
19:29 Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
19:30 akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa.
19:31 Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, `Bwana ana haja naye."`
19:32 Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia.
19:35 Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu.
19:36 Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
19:37 Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona;
19:38 wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!"
19:39 Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!"
19:40 Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti."
19:41 Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia
19:42 akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako.
19:43 Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote.
19:44 Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa."
19:45 Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara
19:46 akisema, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala`; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi."
19:47 Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza,
19:48 lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.