1:16 Yakobo alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.
1:17 Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.
1:18 Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
1:19 Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri.
1:20 Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
1:21 Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao."
1:22 Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:
1:23 "Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi").
1:24 Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani.
1:25 Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.