3:1 Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea:
3:2 "Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia."
3:3 Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni vijia vyake."`
3:4 Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.
3:5 Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea,
3:6 wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.
3:7 Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mnaweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?
3:8 Onyesheni basi kwa matendo, kwamba mmetubu kweli.
3:9 Msidhani kwamba mtaweza kujitetea kwa kusema, `Baba yetu ni Abrahamu!` Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.
3:10 Basi, shoka liko tayari kuikata mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri, utakatwa na kutupwa motoni.
3:11 Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonyesha kwamba mmetubu. Lakini yule anayekuja baada yangu ana uwezo kuliko mimi. Mimi sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
3:12 Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika." ic
3:13 Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye.
3:14 Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, "Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe."
3:15 Lakini Yesu akamjibu, "Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka." Hapo Yohane akakubali.
3:16 Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na ghafla mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake.