12:1 Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
12:2 Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.
12:3 Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.
12:4 Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.
12:5 Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
12:6 Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
12:7 Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.
12:8 Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.
12:9 Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.
12:10 Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima.
12:11 Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
12:12 Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima.
12:13 Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.
12:14 Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani.
12:15 Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia.
12:16 Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana.
12:17 Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote.
12:18 Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.
12:19 Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana."
12:20 Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake."