2:1 Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea haidhuru wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu.
2:2 Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki.
2:3 Lakini wewe, rafiki, unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo bali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu?
2:4 Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?
2:5 Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajilundikia adhabu kwa Siku ile ambayo ghadhabu ya Mungu na hukumu zake za haki vitadhihirishwa.
2:6 Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
2:7 Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uzima wa milele.
2:8 Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
2:9 Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
2:10 Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
2:11 Maana Mungu hambagui mtu yeyote.
2:12 Wale wanaotenda dhambi bila kuijua Sheria ya Mose wataangamia ingawaje hawajui Sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua Sheria watahukumiwa kisheria.
2:13 Mtu hafanywi kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuisikia Sheria, bali kwa kuitii Sheria.
2:14 Mathalan: watu wa mataifa mengine hawana Sheria ya Mose; lakini kila wanapotimiza matakwa ya Sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha Sheria ingawa hawaijui Sheria.
2:15 Mwenendo wao unaonyesha kwamba matakwa ya Sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea.
2:16 Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.
2:17 Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia Sheria na kujivunia kuwa wa Mungu;
2:18 kwa njia ya Sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema;
2:19 wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani;
2:20 unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika Sheria picha kamili ya elimu na ukweli.
2:21 Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba.
2:22 Unasema: "Msizini," na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu.
2:23 Kwa kujigamba ati unayo Sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja Sheria unamdharau Mungu?
2:24 Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu ninyi Wayahudi!"
2:25 Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii Sheria. Lakini kama unaivunja Sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa.
2:26 Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya Sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa.
2:27 Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja Sheria, ingawaje unayo maandishi ya Sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii Sheria ingawa hawakutahiriwa.
2:28 Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili.