1:1 Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
1:2 Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
1:3 Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
1:4 Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
1:5 Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
1:6 Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
1:7 ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
1:8 Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
1:9 Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
1:10 Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.
1:11 Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
1:12 Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
1:13 Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
1:14 Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
1:15 Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: `Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa."`
1:16 Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
1:17 Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
1:18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
1:19 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?"
1:21 Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!"
1:22 Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma."
1:23 Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: `Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana."`
1:26 Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
1:27 Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake."
1:28 Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng`ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
1:29 Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
1:30 Huyu ndiye niliyesema juu yake: `Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!`
1:31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua."
1:32 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
1:33 Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: `Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.`
1:34 Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu."
1:35 Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
1:36 Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu."
1:38 Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?"
1:39 Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
1:40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
1:41 Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo).
1:42 Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.")
1:43 Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, "Nifuate."
1:44 Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
1:45 Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti."
1:46 Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone."
1:47 Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake."
1:48 Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona."
1:49 Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!"
1:50 Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya."
1:51 Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.