2:1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo,
2:2 naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
2:3 Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
2:4 Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado."
2:5 Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni."
2:6 Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha.
2:7 Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu.
2:8 Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu."
2:9 Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
2:10 akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!"
2:11 Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
2:12 Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.
2:13 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
2:14 Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng`ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
2:15 Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng`ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.
2:16 Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
2:17 Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua."
2:18 Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
2:19 Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu."
2:20 Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
2:21 Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake.
2:22 Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu.
2:23 Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya.
2:24 Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.
2:25 Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.