10:1 Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang`anyi.
10:2 Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
10:3 Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
10:4 Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
10:5 Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake."
10:6 Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
10:7 Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
10:8 Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang`anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza.
10:9 Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
10:10 Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili.
10:11 "Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
10:12 Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.
10:13 Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu.
10:15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
10:16 Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
10:18 Hakuna mtu anayeninyang`anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."
10:19 Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.
10:20 Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?"
10:21 Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"
10:22 Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi.
10:23 Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.
10:24 Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi."
10:25 Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
10:26 Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
10:28 Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
10:29 Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
10:30 Mimi na Baba, tu mmoja."
10:31 Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.
10:32 Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?"
10:33 Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu."
10:34 Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: `Mimi nimesema, ninyi ni miungu?`
10:35 Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.
10:36 Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: `Unakufuru`, eti kwa sababu nilisema: `Mimi ni Mwana wa Mungu?`
10:37 Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini.
10:38 Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."
10:39 Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
10:40 Yesu akaenda tena ng`ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.
10:41 Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa."