11:1 Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake.
11:2 Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.)
11:3 Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!"
11:4 Yesu aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe."
11:5 Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro.
11:6 Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
11:7 Kisha akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!"
11:8 Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?"
11:9 Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
11:10 Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake."
11:11 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha."
11:12 Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona."
11:13 Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.
11:14 Basi, Yesu akawaambia waziwazi, "Lazaro amekufa;
11:15 Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake."
11:16 Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, "Twendeni nasi tukafe pamoja naye!"
11:17 Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne.
11:18 Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu.
11:19 Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao.
11:20 Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani.
11:21 Martha akamwambia Yesu, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!
11:22 Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa."
11:23 Yesu akamwambia, "Kaka yako atafufuka."
11:24 Martha akamjibu, "Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho."
11:25 Yesu akamwambia, "Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi:
11:26 na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?"
11:27 Martha akamwambia, "Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni."
11:28 Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani, "Mwalimu yuko hapa, anakuita."
11:29 Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu.
11:30 Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki.
11:31 Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
11:32 Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwabia, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!"
11:33 Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni.
11:34 Kisha akawauliza, "Mlimweka wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo uone."
11:35 Yesu akalia machozi.
11:36 Basi, Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda!"
11:37 Lakini baadhi yao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?"
11:38 Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.
11:39 Yesu akasema, "Ondoeni hilo jiwe!" Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, "Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!"
11:40 Yesu akamwambia, "Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?"
11:41 Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, "Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza.
11:42 Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma."
11:43 Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: "Lazaro! Toka nje!"
11:44 Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, "Mfungueni, mkamwache aende zake."
11:45 Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu wakamwamini.
11:46 Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu.
11:47 kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno.
11:48 Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!"
11:49 Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, "Ninyi hamjui kitu!
11:50 Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?"
11:51 Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao;
11:52 na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika.
11:53 Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu.
11:54 Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
11:55 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo.
11:56 Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika pamoja Hekaluni wakaulizana, "Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?"