16:1 "Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu.
16:2 Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu.
16:3 Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi.
16:4 Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
16:5 Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: `Unakwenda wapi?`
16:6 Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.
16:7 Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.
16:8 Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.
16:9 Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;
16:10 kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;
16:11 kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.
16:12 "Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.
16:13 Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja.
16:14 Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
16:15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
16:16 "Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!"
16:17 Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?` Tena anasema: `Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"`
16:18 Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: `Bado kitambo kidogo?` Hatuelewi anaongelea nini."
16:19 Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?`
16:20 Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
16:21 Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani.
16:22 Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.
16:23 Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni.
16:24 Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.
16:25 "Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba.
16:26 Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu;
16:27 maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
16:28 Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba."
16:29 Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo.
16:30 Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu."
16:31 Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa?
16:32 Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami.