Bad Advertisement?

News / Reviews:
  • World News
  • Movie Reviews
  • Book Search

    Are you a Christian?

    Online Store:
  • Visit Our eBay Store



  • SWAHILI BIBLIA - JOHN 17

    JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


    17:1 Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, "Baba, saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza.

    17:2 Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wote hao uliompa.

    17:3 Na uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma.

    17:4 Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa nifanye.

    17:5 Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu.

    17:6 "Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako.

    17:7 Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako.

    17:8 Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma.

    17:9 "Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea hao ulionipa, maana ni wako.

    17:10 Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana ndani yao.

    17:11 Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja.

    17:12 Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule aliyelazimika kupotea ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia.

    17:13 Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu.

    17:14 Mimi nimewapa neno lako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.

    17:15 Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu.

    17:16 Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.

    17:17 Waweke wakfu kwa ukweli; neno lako ni ukweli.

    17:18 Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni;

    17:19 na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu katika ukweli.

    17:20 "Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao.

    17:21 Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma.

    17:22 Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi tulivyo mmoja;

    17:23 mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda wao kama unavyonipenda mimi.

    17:24 "Baba! Nataka wao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu.

    17:25 Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua kwamba wewe ulinituma.

    17:26 Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao.

    IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

    God Rules.NET
    Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine