15:1 Siku moja, watoza ushuru na wahalifu wengi walikwenda kumsikiliza Yesu.
15:2 Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kunung`unika: "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao."
15:3 Yesu akawajibu kwa mfano:
15:4 "Hivi, mtu akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate.
15:5 Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha.
15:6 Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake akiwaambia, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.`
15:7 Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. ic
15:8 "Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, aifagie nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate.
15:9 Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake akisema, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.`
15:10 Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu."
15:11 Yesu akaendelea kusema, "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili.
15:12 Yule mdogo, alimwambia baba yake: `Baba, nipe urithi wangu.` Naye akawagawia mali yake.
15:13 Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo.
15:14 Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika.
15:15 Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.
15:16 Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu.
15:17 Alipoanza kupata akili akafikiri: `Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa?
15:18 Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.
15:19 Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.`
15:20 Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu.
15:21 "Mwanawe akamwambia: `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.`
15:22 Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: `Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu!
15:23 Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea!
15:24 Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.` Wakaanza kufanya sherehe.
15:25 "Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani akasikia vifijo na ngoma.
15:26 Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: `Kuna nini?`
15:27 Huyo mtumishi akamwambia: `Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.`
15:28 Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie.
15:29 Lakini yeye akamjibu: `Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu!
15:30 Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.`
15:31 Baba yake akamjibu: `Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako.
15:32 Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."`