16:1 Yesu aliwaambia wanafunzi wake: "Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake.
16:2 Yule tajiri akamwita akamwambia: `Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.`
16:3 Yule karani akafikiri: `Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu.
16:4 Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.`
16:5 Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmoja mmoja, akamwambia yule wa kwanza: `Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?`
16:6 Yeye akamjibu: `Mapipa mia ya mafuta ya zeituni.` Yule karani akamwambia: `Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.`
16:7 Kisha akamwuliza mdeni mwingine: `Wewe unadaiwa kiasi gani?` Yeye akamjibu: `Magunia mia ya ngano.` Yule karani akamwambia: `Chukua hati yako ya deni, andika themanini.`
16:8 "Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga."
16:9 Naye Yesu akaendelea kusema, "Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, mweze kupokewa nao katika makao ya milele.
16:10 Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa.
16:11 Kama basi, ninyi si hamjawa waaminifu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli?
16:12 Na kama hamjakuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe?
16:13 "Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali."
16:14 Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu.
16:15 Hapo akawaambia, "Ninyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.
16:16 "Sheria na maandishi ya manabii vilikuweko mpaka wakati wa Yohane mbatizaji. Tangu hapo, Ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu.
16:17 Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya Sheria kufutwa.
16:18 "Yeyote anayemwacha mke wake na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.
16:19 "Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau, na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku.
16:20 Kulikuwa pia na maskini mmoja jina lake Lazaro, aliyekuwa amejaa vidonda na alikuwa analazwa mlangoni pa nyumba ya huyo tajiri.
16:21 Lazaro alitamani kula makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kulamba vidonda vyake!
16:22 "Ikatokea kwamba huyo maskini akafa, malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa.
16:23 Huyo tajiri, alikuwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye.
16:24 Basi, akaita kwa sauti: `Baba Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.`
16:25 Lakini Abrahamu akamjibu: `Kumbuka mwanangu, kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa.
16:26 Licha ya hayo, kati yetu na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, wala wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.`
16:27 Huyo aliyekuwa tajiri akasema: `Basi baba, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu,
16:28 maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.`
16:29 Lakini Abrahamu akamwambia: `Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.`
16:30 Lakini yeye akasema: `Sivyo baba Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka wafu na kuwaendea, watatubu.`
16:31 Naye Abrahamu akasema: `Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka wafu."`