7:1 Baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu.
7:2 Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa.
7:3 Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo.
7:4 Tena hawali kitu chochote kutoka sokoni mpaka wamekiosha kwanza.*fc* Kuna pia desturi nyingine walizopokea kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.
7:5 Basi, Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, "Mbona wanafunzi wako hawayajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?"
7:6 Yesu akawajibu, "Wanafiki ninyi! Nabii Isaya alitabiri ukweli juu yenu alipoandika: `Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno matupu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
7:7 Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.`
7:8 Ninyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu."
7:9 Yesu akaendelea kusema, "Ninyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu.
7:10 Maana Mose aliamuru: `Waheshimu baba yako na mama yako,` na, `Anayemlaani baba au mama, lazima afe.`
7:11 Lakini ninyi mwafundisha, `Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani ni zawadi kwa Mungu),
7:12 basi, halazimiki tena kuwasaidia wazazi wake.`
7:13 Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo."
7:14 Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, "Nisikilizeni nyote, mkaelewe.
7:15 Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu toka nje ambacho chaweza kumtia mtu najisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu najisi."*fd*
7:16 missing
7:17 Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano.
7:18 Naye akawaambia, "Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi,
7:19 kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?" (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.)
7:20 Akaendelea kusema, "Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi.
7:21 Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,