8:1 Wakati huo umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
8:2 "Nawahurumia watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu, wala hawana chakula.
8:3 Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali."
8:4 Wanafunzi wake wakamwuliza, "Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?"
8:5 Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Nao wakamjibu, "Saba."
8:6 Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.
8:7 Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.
8:8 Watu wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki yaliyosalia wakajaza makapu saba.
8:9 Nao waliokula walikuwa watu wapatao elfu nne. Yesu akawaaga,
8:10 na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.
8:11 Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka awafanyie ishara kuonyesha anayo idhini kutoka mbinguni.
8:12 Yesu akahuzunika rohoni, akasema, "Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote!"
8:13 Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng`ambo ya pili ya ziwa.
8:14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua.
8:15 Yesu akawaonya, "Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode."
8:16 Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, "Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate."
8:17 Yesu alitambua hayo, akawaambia, "Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imeshupaa?
8:18 Je, Mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki
8:19 wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu elfu tano? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki ya makombo?" Wakamjibu, "Kumi na viwili."
8:20 "Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu elfu nne, mlikusanya makapu mangapi ya makombo?" Wakamjibu, "Saba."
8:21 Basi, akawaambia, "Na bado hamjaelewa?"
8:22 Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu mmoja, wakamwomba amguse.
8:23 Yesu akamshika mkono huyo kipofu, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, "Je, unaweza kuona kitu?"
8:24 Huyo kipofu akatazama, akasema, "Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea."
8:25 Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.
8:26 Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, "Usirudi kijijini!"
8:27 Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema mimi ni nani?"
8:28 Wakamjibu, "Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Eliya na wengine mmojawapo wa manabii."
8:29 Naye akawauliza, "Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?" Petro akamjibu, "Wewe ndiwe Kristo."
8:30 Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.
8:31 Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake: "Ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Atauawa na baada ya siku tatu atafufuka."
8:32 Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Basi, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea.
8:33 Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, "Ondoka mbele yangu, Shetani! Fikira zako si za kimungu ila ni za kibinadamu!"
8:34 Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
8:35 Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa.
8:36 Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake?
8:37 Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake?